1 Corinthians 1:19-31

19 aKwa maana imeandikwa:

“Nitaiharibu hekima ya wenye hekima,
na kubatilisha akili ya wenye akili.”
20 bYuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu? 21 cKwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. 22 dWayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima. 23 eLakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi. 24 fLakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Kristo ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu. 25 gKwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.

26 hNdugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 iLakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 jAlivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 kili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30 lBali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi. 31 mHivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

Copyright information for SwhNEN